SHEREHE

Kila chenye kurutub

UBUYU UNAUZWA


YALETAYO FURAHA NA AMANI KATIKA NDOA

Image result for furaha ya ndoa

Kutiana Moyo na Kutakiana Mema
Jifunze kumtia moyo na kumtakia mema mwenzako. Mpenzi wako anapofanya vizuri mpongeze iwe mbele za watu au hata unapokua nae peke yenu. Mruhusu mpenzi wako ajue kuwa una mkubali katika kila afanyalo. Kadiri tunavyo wainua wapenzi wetu ndivyo wanavyotuthamini na kutunyanyua na sisi pia.

Kutokuwa na Kiburi na Majivuno
Mtu mwenye kiburi huwa na majivuno kwa kuamini kwamba hakuna kinachoweza kumbabaisha. Daima kila unaloelekezwa hufanyi, badala yake unakuwa mtu katika kupuuzia mambo. Mfano: Unaweza ukawa mmepanga miadi wewe na mwenzi wako mkutane mahali, lakini unaamua kutokwenda bila sababu ya msingi.

Mpo katika maongezi ya faragha, mwenzio anajaribu kukuelewesha katika maeneo ambayo huwa unakosea, lakini badala ya kupokea ukweli, unaamua kunyamaza kimya, kufoka na kumjibu vibata halafu unamkunjia sura kana kwamba anachokwambia si ukweli bali ni uzushi tu.

Tabia hii ukiwa nayo ni rahisi kuachwa kwa sababu hakuna siku ambayo mpenzi wako atakuwa anajisikia faraja kuwa na wewe.

Usafi
Usafi ni jambo muhimu sana katika kujihakikishia tunafurahia mapenzi na kupendana. Usafi wa Mwili na mazingira ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku.

Tusiruhusu harufu za ajabu ajabu iwe ya mwili au mazingira hasa zile zinazoweza kuharibu starehe ya tendo la ndoa. Tujitahidi kuwa wasafi kwa kufanya usafi wa mazingira yanayotuzunguka (ndani na njeya nyumba), kuoga mara kwa mara hasa kabla hatujakutana na wenza wetu, tusafishe sehemu zote ambazo tunahisi zina tabia ya kutoa harufu, tunyoe nywele za kwenye makwapa na sehemu za siri kwani nazo zinachangia kuleta harufu na mba wakati mwingine.

Pia tujitahidi kupaka mafuta au manukato yenye harufu nzuri ili kujenga hali ya mvuto kwa wale wanaotupenda.

Heshima na adabu
Unapokuwa kwenye uhusiano jitahidi kumpenda mwenzi wako kwa hali yoyote na usonyeshe dharau kwake au hata kwa marafiki zake au ndugu zake au hata wengineo. Hakuna mtu anayependa mtu mwenye dharau hata awe nani.

Na hii huwa mara nyingi inatokea pale mmojawapo kati ya wanaopendana akimzidi mwenzake uwezo iwe kwa cheo, pesa,uzuri au hata akili na mara nyingi sana inatokea kwa wasichana pale wanapokuwa wapo juu ya wapenzi wao kiuwezo.

Wasichana wanatakiwa kutambua kuwa linapokuja suala la mahusiano ya kimapenzi au ndoa uzuri sio kigezo cha pekee cha kumfanya mwanamke aolewe. Ingekuwa hivyo basi wanawake wote warembo wangekuwa ndani ya ndoa leo hii. Hii Inamaanisha kuwa hata ukiwa mzuri hutakiwi kujisahau ukaona umeshafika...Utapotea ukileta dharau kwa uzuri wako au uwezo ulionao.

Unyenyekevu
Unyenyekevu ni mbolea ya mapenzi, kinyume chake ni sumu, ndiyo maana ubishi ni sumu katika uhusiano wa kimapenzi. Changamoto hii, kama ingekuwa inaeleweka vizuri na kuzingatiwa inavyotakiwa, pengine kusingekuwa na watu wanaotengana.

Binadamu tumeumbwa na udhaifu, kwahiyo kukosea siyo vibaya kwa kuwa ni sehemu ya maisha yetu. Pamoja na kulifahamu hilo, lakini wengi wetu huwa hatutaki kukubali ukweli katika yale tunayokuwa tumekosea.

Tunataka tushinde kwa hoja hata kwenye mambo ambayo tunastahili kuwaomba radhi wapenzi wetu. Tabia ya namna hiyo huwaumiza wenzetu moyoni kwa sababu wao huamini wamekosewa, kwahiyo hutarajia angalau kuombwa msamaha.

Fikiria mpenzi wako amekufanyia kosa ambalo wewe unaliona kama ni kubwa, unamuweka chini unaongea naye, lakini mwenzako anakuruka futi hamsini. Hataki kukubali kosa na zaidi anataka mbishane mpaka makoo yawakauke. Embu chukuliwa wewe ndo ungekuwa umefanyiwa hivi na mpenzi wako, ungejisikiaje?

Maumivu ambayo unahisi wewe ungeyapata endapo ungefanyiwa kitendo kama hicho, basi ujue kuwa ndiyo anayopata mwenzako kutokana na tabia yako ya kutotaka kukubali ukweli.

Uvumilivu
Kama mpo kwenye mapenzi na mmeamua kupendana kwa shida na raha basi haitakiwi mmoja wenu kuwa na tama na kukosa uvumilivu hata kwa yale mambo yanayoweza kuzuilika. Hakuna mapenzi duniani yanayoweza kushamiri bila ya uvumilivu. Usipokuwa na moyo wa uvumilivu katika mapenzi basi kila mtu utamuona hafai na kila siku utakuwa mtu wa kuanzisha mahusiano mapya.

Mahusiano yaliyodumu si kwa kuwa wahusika hawakoseani au makosa wanayokoseana ni madogo sana, hapana. Kila binaadamu ana mapungufu yake. Wote ambao mahusiano yao yamedumu, wanakoseana ila tofauti yake na wengine ni kwamba busara na uvumilivu huwa msingi wa mapenzi yao na ndiyo maana tunaona wanadumu mpaka leo.

Ni binaadamu gani ambaye unaweza kuishi naye mda mrefu na msikoseane? Hakuna binadamu wa aina hiyo.

Mapenzi yasiyo kuwa na uvumilivu ndani yake hayana maisha marefu. Kwa sababu binadamu ni kiumbe dhaifu na wakati wowote anaweza kukosea.

Uaminifu
Hakuna kitu kinauma katika uhusiano wa kimapenzi kama kugundua kuwa yule unayempenda tena kwa dhati na kumjali kwa kila kitu, ana mtu mwingine zaidi ya wewe.

Huwa inauma sana na mara nyingi huwa inasababisha hata wengine kuweza kuondoka kwenye mahusiano hata kama walikuwa bado wanapenda pale walipo. Hakuna binadamu anayependa kushea mapenzi.

Kamwe usiuumize moyo wa mtu anayekupenda kwa dhati, usimfanye ajute kuwa nawe maishani na usimfanye anung'unike kwa unayomtendea. Unaweza kuona ni ujanja lakini ipo siku utahitaji mapenzi ya kweli kwa mwingine na hutayapata. Laana ya mapenzi ipo. Ukimuumiza mtu ambaye anakupenda kwa dhati, ipo siku nawe utaumizwa tu.

Msamaha
Kamwe tusiache maumivu na machungu yatawale mahusiano yetu. Lazima tujifunze kuwasamehe tuwapendao na kujisamehe sisi pia. Kutofautiana katika mahusiano kupo sana, na lazima tuwape tuwapendao nafasi ya kuelezea vile vinavyowaudhi dhidi yetu. Kila hisia za mmoja wetu zinaumuhimu. Huwezi kuona vile ulivyo, mruhusu mwenzako akuambie yanayo muumiza na msameheane.

Huruma na Kujali
Ndani ya uhusiano, huruma ni kitu muhimu sana, kwa sababu mtu mwenye anayejali na mwenye huruma kamwe hawezi kumfanyia mwenzake mabaya.

Uhusiano wa kimapenzo wenye kujaliana na kuoneana huruma, hudumu milele na kutenganishwa na kifo. Asiyekuwa na huruma, hufanya jambo lolote bila kujali maumivu ya mwenzake.

Tendo la ndoa
Kufanya mapenzi baina ya wawili wapendanao hasa kama wameoana ni moja ya chachu ya ndoa ambayo husaidia kushikilia na kuimarisha ndoa hiyo endapo ikatumika vizuri na kwa wote kufurahia hasa kwa wale ambao hushirikiana katika kila kitu.

Bila ya tendo la ndoa hakuna ndoa. Lakini pia izingatiwe kuwa kufurahia tendo la ndoa haiji kirahisi, ni lazima ijengwe na kuimarishwa na upendo, kujituma, utundu na ububunifu.

Hivyo ili uweze kumridhisha vyema mwenzi wako ni vyema kwa wana ndoa wakawa waanazungumzia kuhusu tendo la ndoa ili kubaini kama mwenzi wako kama anaridhika katika tendo au la, kitu kipi hupendi, kitu gani unapenda, wapi unapenda kuguswa, vipi unapenda kukunwa, na ni kitu gani ambacho kinakupandisha mzuka n.k huku wewe mwenzie ukiwa mtundu katika kuhakikisha unavumbua maeneo mengine ambayo hata yeye hakujua kuwa anaweza pata raha hiyo ambayo anaipata kwa wakati huo.

Hitimisho
Yapo mambo mengi sana ambayo yakifanywa yanaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ndoa na kuifanya ndoa hiyo iwe ya amani, upendo na furaha. Lakini haya niliyoyaandika ni baadhi tu na ni mambo ya msingi ambayo kila mwanandoa ambaye anatamani kuwa na ndoa yenye amani, upendo na furaha anapaswa kuayafuata kwa sababu hapa ndipo msingi wa upendo ulipo.

Jee unahisi umeshaanza kumchoka mumueo au mkeo?

Image result for MATATIZO KATIKA NDOA


Imeandikwa na Shams Elmi (Abu 'Ilmi)

Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti. Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.

Utoto wa Ndoa:

Wengine hukiita kipindi hiki (Honey Moon) mwezi wa asali, kipindi cha raha, utulivu, mapenzi, maelewano baina ya wanandoa. Si lazima kiwe mwezi mmoja kama watu wengi wanavyoamini, bali kinaweza kikawa chini ya mwezi mmoja au zaidi ya mwezi mmoja.


Ujana wa Ndoa:

Hiki ni kipindi kinachofuatia baada tu ya utoto wa ndoa, ni kipindi ambacho kila mmoja miongoni mwa wanandoa anakuwa tayari ameshamtambua mwenzake katika shaksia yake (personality) kwa maana ya jinsi anavyoangalia mambo, jinsi anavyofikiri, mitazamo yake, mielekeo yake na matarajio yake.

Uzee wa Ndoa:

Kipindi hiki ni kipindi ambacho wanandoa wanakuwa tayari wameishaingia katika majukumu ya kulea kwa kupata matunda ya ndoa yao ambayo ni mtoto au watoto.

Kuchokana kwa wanandoa ni tatizo ambalo linatokea kwa familia nyingi, na kusababisha migogoro mingi na hata kufikia familia kuvunjika au kuishi kwa ajili tu ya kulea watoto na si vinginevyo.

Utakuta katika baadhi ya familia, Baba na Mama wanaishi katika nyumba moja, ukiwaona utadhani ni mume na mke wanaopendana, kumbe wanaishi kwa ajili tu ya kuwalea watoto wao na kuogopea maneno ya watu, hali hii ni hali ya talaka ya kimapenzi (emotional Divorce) na ni hali mbaya ambayo mara nyingi humpa msukumo mwanamume wa kuoa mke wa pili katika harakati za kutafuta utulivu na sehemu ya kukimbilia

Tatizo hili la kuchokana kwa wanandoa linasababishwa na wanandoa wote wawili kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki za mume na mke.

Hivyo basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao, na hapa nitajaribu kujadili baadhi ya visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa ndoa au kuchokana visababishi ambavyo huwa vinadharaulika na kuonekana vitu vidogo vidogo hususan kwa wanawake wengi.

a) Kuzoeana: kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususan kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla. Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana, kwa mfano: siku za utoto wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu, mapokezi yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini. Lakini baada ya kuzoeana yote hayo hubadilika, mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumuonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku, mambo ya Hinna, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini na sio nyumbani. Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau.

b) Mazungumzo: Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha , aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana. Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake. Kwa mfano: Mwanamke ambaye kila anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu wakati wote. Mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.

c) Kusomana Tabia: ni udhaifu mkubwa kwa wanandoa ambao wana mwaka mmoja katika ndoa yao wakawa bado hawajasomana tabia, au wakawa wameishasomana tabia, lakini kila mmoja akawa anataka tabia zake ndio ziwe dira. Kwa mwanamke mwenye busara na mwenye kuithamini ndoa yake, husoma tabia za mumewe na kuangalia jinsi gani anavyoweza kuzioanisha na zile zake ili kuepusha migongano, aidha hutafuta fursa muafaka ya kumkinaisha mumewe juu ya fikra fulani au tabia fulani ambayo yeye haridhiki nayo. Ni muhimu kwa mwanaume vilevile kuzisoma tabia za mke wake, vitu gani vinamuudhi, na vitu gani vinamfurahisha.

d) Kutamka na kudhihirisha mapenzi: Ni muhimu sana kwa wanandoa ili kuyaimarisha mapenzi yao yasiote mvi, kutamkiana hisia zao za kupendana bila utangulizi wowote, kwa mume au mke kumwambia mwenzake NAKUPENDA kuna athari nzuri katika nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama.

e) Kupeana zawadi: Zawadi ni njia nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako na nafasi ya mwenzako katika maisha yako, na zawadi ambayo mtu huitoa kwa mwenzake bila ya utangulizi au mnasaba maalum huleta athari njema na huimarisha mapenzi. Na katika zoezi hili la kupeana zawadi, ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda mwengine ili zawadi iwe na athari inayotarajiwa, na iwe ni zawadi maalum kwa mlengwa, isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo, kwa mfano, si vema kwa mwanamme kumletea mkewe zawadi ya sufuria, microwave, pazia, Dinner set, hiyo haitaitwa zawadi, lakini ni juu yake kumletea manukato ayapandayo, hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu, na vitu ambavyo ni maalumu kwa matumizi yake binafsi. Hali kadhalika kwa mwanamke kumzawadia mumewe achunge vigezo hivyo.

f) Kualikana vyakula: Inaweza kushangaza kuwa vipi wanandoa wataalikana chakula wakati wenyewe ni mume na mke, na ni lazima wale pamoja?! Ni vema ikaeleweka kuwa, kubadili mazingira na kufanya vitu makhsusi kwa kushtukizana, huwafanya wanandoa kutozoeana na kuchokana, kwani maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja kila siku humfanya mtu kuyachoka, ni vema wanandoa na hasa mwanamke kuwa mbunifu katika kuyapaka rangi mpya maisha yao kwa kubuni vitu vitakavyo tia ladha mpya katika nyumba, njia mojawapo ni hiyo ya kumualika chakula maalum mumewe peke yake, na hata kama itamlazimu kununua au kuagiza aina tofauti ya chakula basi afanye hivyo, na ampe mwaliko mumewe wa kutokosa kuhudhuria katika mnasaba huo. Aidha mwanamume naye anaweza kumualika mkewe katika hoteli ya heshima mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya kujikumbusha mambo mazuri yaliopita.

g) Kubadilisha mpangilio wa nyumba: Wanawake wengi huwalalamikia waume zao kwa kutopenda kukaa nyumbani na badala yake kumaliza muda wao kwenye migahawa na kwa marafiki zao. Mke mwerevu huwa anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba, kwani mazingira ya nyumba yanapokuwa ni yale yale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu, kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa basi rangi ni zilezile, hali hii humfukuza mwanamume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala tu, na huu ndio mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba.

h) Usafi wa mwili na mavazi: Moja miongoni mwa mambo yanayokera kwa wanandoa ni uchafu wa mmoja wao, uchafu ni sifa isiyovumilika hususan kwa mwanamke, baadhi ya wanawake hudhani kuwa manukato, vipodozi ndio usafi, utakuta anapitisha masiku bila kuoga kikamilifu, bali anapitisha pitisha maji na sabuni tu katika maeneo fulani, kisha kujijaza manukato, lotion na mafuta mengine, bila kuelewa kuwa, anapokuwa karibu zaidi na mumewe harufu ya asili hujitokeza na kuleta mchanganyiko wa harufu mbaya, hali kama hii si rahisi kwa mwanaume mstaarabu kuizungumzia kwa mkewe, atakaa nayo na atavumilia, lakini mwisho wake ni kumchoka mke huyu. Wanaume nao hudhani kuwa kwao wanaume ndio wamepewa kibali cha kuwa wachafu, kwa mfano wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho, na wengine wana matatizo sugu ya kunuka miguu, huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi, aidha baadhi ya wanaume hawana vionjo katika mavazi yao, na jinsi wanavyojiweka, jambo ambalo linaweza kumsababishia mke maudhi, na hata kujihisi aibu kunasibishwa na mume wake.

i) Kufanya Ibada kwa pamoja: Nguzo muhimu na mhimili wa maisha ya ndoa ni kumcha Mungu/Allaah, Sala za usiku humkurubisha mja karibu zaidi na Mungu, hivyo mume na mke kuhimizana kufanya ibada hii pamoja huwazidishia imani na mapenzi baina yao na kuifanya ndoa yao kuwa imara zaidi.

MAMBO 8 YA KUZINGATIA KABLA YA NDOA


MUTURI Vitu 8 Vya Kuwa Macho Kabla Ya Ndoa.
Ndoa ni ktu cha muhimu sana kinachobadilisha maisha ya watu wawili wanapoamua kuishi  kwa pamoja.
Pale unaposema , Nakubali.
Maisha hubadilika palepale, huwezi tena kuwa  yule mtu wa kwanza.
Ndiooo!!.
huwezi kutengana na mwenzio na kwenda kwa mwingine.
Kwa sababu unapoolewa, unapooa  huyo mtu anakuwa ni sehemu ya mwili wako na ni sehemu ya maisha yako, kuanzia hapo hadi siku ya kufa, lazima ulielewe hilo mapema. kwa hio nakuletea hapa vitu 8  vya kuwa makini kabla ya ndoa.
1.Lazina kutambua kama wote mko sahihi.
Mara nyingi watu hujikuta wameoana , si kwa ajili ya kupendana kwa dhati , ni vile walikuwa wakikutana kimwili kawaida, kuridhishana kawaida. lakini watu hawa hufika wakati  hugundua kuwa hawakutakiwa kuoana. ndoa inakuwa haina amani tena. hata kama walikuwa wanafurahia vipi hilo tendo ,  hawakuwa sahihi kila mmoja.
Kwa maana hii basi , mimi naamini kwamba ni vizuri kufanya tendo hilo ukiwa ndani ya ndoa, kuliko kutengeneza  mahusiano kwa ajili ya kufurahishana  halafu basi. labda kama ni urafiki tu  au ni mazoea ya kawaida.
Jaribu sasa kuangalia hisia za mwenzio, endapo hutafanya nae kitu ,   atakuaje? mnaweza kuelewana? , je unaweza kucheza nae , kufanya vitu vingi  bila ya kufanya tendo la ndoa? bado atakuwa na mapenzi na wewe. maana kuna mwingine nia yake ni moja tu kwako.  washa taa yako ya ndani utagundua kama huyo ni wako ama sio.
friends2504 Vitu 8 Vya Kuwa Macho Kabla Ya Ndoa.
2.Ni lazima kujua mambo yake ya mwanzo kabla ya kuja kwako.
Kwa swali hili sisemi mapenzi mlionayo, au ni mazoea gani mko nayo, hapana. kuna vitu ambavyo havisemwi kati yenu. hasa mahusiano yaliopita. usidanganye sema ukweli, ulikuwa na mke ukamwacha, uliolewa ukaachika mapema hata kabla ya mwezi , sema mapema  . una mtoto ulizaa kabla sema.  kuna msichana ulikuwa nae akakuumiza sema,  isije baadae  ukajulikana  hivyo vitu ni bora ukisema  inaokoa mambo mengi.
Naesema hivyo kwa sababu , usipokuwa muwazi itakugharimu baadae, hata kama uliwahi kubakwa inabidi kusema, hutapata furaha ukikaa nalo.
3.Chunguza kama mnaheshimiana.
Ndoa haiwezi kuwa nzuri kama hakuna heshima kati yenu,Heshima nin nini basi,  ni kuona kuwa mwenzio anastahili, ni muhimu kwako,  ni maalumu sana kwako, kitu adimu  cha thamani, yupo kwa ajili yako, unatumia muda mwingi  kwa ajili yake, kumpa kipaumbele. kama wewe ni mkweli sema ndio. unamheshimu huyo mtu. na kama sio chukua hatua nyingine.
DSC_00412-1024x684 Vitu 8 Vya Kuwa Macho Kabla Ya Ndoa.
4.Angalia kama anakuona wewe ni peke yako. wa kwake tu.
Tatizo kubwa linalosababisha ndoa nyingi kuvunjika ni usaliti . ni hatari sana , na ni kweli sio sahihi. kwenye kiapo  cha ndoa uliahidi kumpenda, kumheshimu na kumfanya awe na furaha kila siku.
Uliahidi kuwa mwaminifu mpaka kufa.
Kama huwezi kutunza hio ahadi , Usioe, usiolewe.
Watu waliooana wanatakiwa kukamilishana wao kila mmoja na hamu zao bila ya msaada wa nje.
Haijalishi utatumia mbinu zipi kutengeneza hilo lakini mtu anaekuoa , unaemuoa lazima  akufanyie vitu hivyo, ili usiweze kuhitaji mtu mwingine.
Je huyo ulie nae anakutimizia hayo? ni mume au mke wa kukutosheleza?.
158660566-e1369108970576-1024x612 Vitu 8 Vya Kuwa Macho Kabla Ya Ndoa.
5.Utanipenda nikiwa mgonjwa na nikiwa mzee?
Usiangukie kwa mtu ambae anatafuta kampani, amechoka kuwa peke yake, anayeonekana amechoshwa na muda. ila angalia uzuri uliopo ndani yake. jiweke mwenyewe kwenye viatu  vyake.mfano mtu ambae ni mgonjwa wa cancer, utakuwa unampenda wakati wote  anaumwa na amepoteza nywele zake zote?
akiwa amezeeka utampenda?
Na kama utampenda mtu kwa sababu yeye ni sex  na ana misuli, au ni mzuri na ana umbo zuri, utakuwa umefeli. huo sio upendo. itaisha kwa muda mfupi .
Hakikisha unampenda mtu jinsi alivyo, penda utu wao, penda jinsi ambavyo wanakufanya uwe na furaha wakati unapokuwa na huzuni.
Wapende kwa kila kitu kinachowafanya wao wawe ni wao.
6.Tunayo nafasi?
usipoteze muda kwa  watu wengine , huoi au huolewi ili uwe kama wao. unaoa au unaolewa ili kuanzisha timu mpya  na tofauti na wengine. wala usifananishe tabia zao na za kwenu, nyie ni tofauti, furahieni vitu kwa pamoja. lakini mwache mwenzako aende  kazini kwake na wewe nenda kazini kwako.
hakuna tatizo kufanya kazi sehemu tofauti. jipeni nafasi, kwa kuaminiana kila mmoja.
7.Angalia kama mnasaidiana.
je, unapokuwa na matatizo , unamwona akiwa mstari wa mbele kukusaidia?,, je anapokuhitaji unakuwepo  kwa wakati?, maswali haya ni muhimu, jifunze kusaida, ni wamoja inabidi kusaidiana, unatumia nguvu nyingi kumuelimisha na kukuelewa au hapana.
chunguza hivi vitu kujua ugumu uko wapi kabla ya kuingia kwenye agano.
ee0a0__couple-moving-into-an-apartment Vitu 8 Vya Kuwa Macho Kabla Ya Ndoa.
8.Ni mambo yapi huwa hakubaliani.
Kuhusu fedha, watoto na familia inabidi kuongelea mapema,kazi zenu, kupanga watoto wangapi, jinsi ya kutunza rasilimali, matumizi ya fedha yote huongelewa kabla..
Ndoa ni hatua muhimu  katika  maisha ya kila mwanadamu, kwa hio uwe makini sana na uchague kwa hekima.
Endapo umeoa au umeoolewa unakaribishwa kuongeza maoni yako, na wale ambao bado karibuni kwa maswali.
shirikisha makala hii rafiki na familia yako.

UMUHIMU WA KUPEANA ZAWADI KATIKA NDOA

Mwanamke anahitaji alama za upendo kutoka kwa mwanaume.
Mwanaume anapompelekea mwanamke (mkewe) zawadi hii hudhihirisha kwamba mwanamke ana thamani na anamjali, mfano zawadi ya maua huonesha kwamba mwanamke ni mrembo na ana uzuri ambao mwanaume anaukubali.

Iwe zawadi kubwa au ndogo zote hutoa maana halisi ya mapenzi, humsaidia mwanamke kufahamu kwamba yeye ni mwanamke special, na kumpa zawadi mwanamke ni njia ya kumpa heshima na thamani ambayo mwanamke huhitaji kutoka kwa mume wake.

Kuna alama nyingi ambazo huonesha kwamba unampenda mke wako moja ni kumpa zawadi mbalimbali kama maua au kadi yenye ujumbe unaoelezea hisia zako kwake nk.
Ni muhimu mwanaume kuwa creative na innovative katika kuhakikisha penzi linazidi kunawiri kila iitwapo leo katika ndoa yako na unajitahidi kutoa hisia zako original pale unampa zawadi au kumwandikia text message (sms) yoyote, kitu cha msingi afahamu kwamba kuna mwanaume anayemjali.

Wanaume wengi huwa wanakuwa wataalamu na wajuzi sana wa kuwapelekea wapenzi wao zawadi motomoto na kadi zenye maneno matamu matamu mwanzo wa mahusiano (uchumba au ndoa) na baada ya muda wanaachana kabisa na hiyo tabia, hili ni kosa kubwa sana ktk masuala ya ndoa, kutoa zawadi hakuzeeki wala ku-expire hudumu na kudumu na kudumu, ni njia muhimu sana ya Kuonesha unamjali mke wako.

Kama ni mwanamke unakumbuka lini mpenzi wako amekuletea zawadi?
Na kama ni mwanaume je, unakumbuka ni lini umempelekea mke wako zawadi?
Eti haya mambo yamepitwa na wakati!
Shauri yako!
Usione vinaelea vimeundwa!

Wanawake wengi kwenye ndoa au mahusiano hujisikia na kujiona hawapendwi na waume zao, hujisikia wanaume hawawajali, ukiangalia kwa undani moja ya sababu ni mwanaume ameacha kumpa zawadi hata ndogondogo, au maneno mazuri (notes) au kadi kama alivyokuwa anafanya mwanzo na kwa sababu ulikuwa unampa na umeacha anajiona humpendi tena, si ulikuwa unampa? sasa imekuwaje? unampelekea nani tena? maana ulikuwa na tabia ya kutoa zawadi.

Kiwango cha attention unayompa mke wako ni alama muhimu ya Kuonesha upendo wako kwake.

Mwanamke hujisikia anapendwa na kwamba unamjali pale mwanaume:-
Unampompa zawadi iwe ndogo au kubwa,
Unapompa zawadi ya kadi yenye maneno mazuri yanayoelezea hisia zako kwake,
Unapomhudumia kwa kumjali,
Unapomsikiliza yeye na kujiona anasikilizwa,
Unapojitolea kumsaidia kazi ndgondogo na mambo ambayo anajisikia upo na yeye,
Unapompa plan za mambo mbalimbali mnayotaka kufanya pamoja kama familia iwe "outing", likizo, business n.k,

Pale unapomuuliza anavyojisikia hasa baada ya kazi au unapohisi emotions zake hazipo sawa,
Unapochukua muda wa ziada kuwa naye na kuwa kwa ajili yake,
Unaposhirikiana naye ktk huzuni au tatizo huku ukimfariji na kumkumbatia,
Unapompa nafasi ya kujisikia huru kwako hata kudeka (si wote)
Unapogundua kwamba amevaa amependeza mavazi na nywele na kumpa sifa anazostahili.
Unapom-surprise na zawadi au notes na
Unapompigia simu ukiwa umesafiri na kumuulizia anaendeleaje na jinsi gani utakuwa unaongea naye na kuwasiliana naye.

SIRI YA ZAWADI KATIKA MAHUSIANO


1. ZAWADI ZINABORESHA MAHUSIANO: 

Umuhimu wakwanza wa Zawadi katika mapenzi ni kuboresha mahusiano. Fahamu kuwa unapompa mpenzi wako zawadi utamfanya ajihisi kama niwapekee kwako hivyo atajiona kama ni mmoja wapo kati ya watu wenye thamani kwako na ataamini kama kweli upo karibu yake na unamjali hivyo hatashindwa kulipa mazuri kwako kwa kukuonesha upendo wa dhati na utamfanya azidishe mapenzi kwako kwani atakua anajua kuwa wewe unamjali na unamuonesha upendo sasa kwanini nayeye asikujali?! Hivyo zawadi yako itakuwa ni njia moja wapo ya kuboresha penzi lako kwa umpendae.

ZAWADI2. ZAWADI ZINAJENGA KUMBUKUMBU KATIKA MAHUSIANO:

Umuhimu wa pili wa zawadi katika mahusiano ni kujenga taswira ya kumbukumbu kwa rafiki, jamaa au mpenzi wako, fahamu kuwa unapompa zawadi inakusaidia wewe kujijenga katika mawazo yake na endapo kama itatokea mkaachana nae basi pindi atakapokuwa anaziona zawadi zako zitamfanya akukumbuke kwa mengi na atahisi kama kuachana nawewe kwake kunatofauti na atajihisi kupoteza vingi toka kwako na kamwe kumbukumbu yako kwake haitofutika kila azionapo zawadi zako.

Mpenzi msomaji wa ukurasa huu napenda nikushauri juu ya zawadi unazotakiwa kumpa mpenzi, rafiki, ndugu au jamaa yako jitahidi pindi unapohitaji kumnunulia zawadi tafuta zawadi ambayo itadumu kama vile nguo, card, maua n.k. Isiwe zawadi ya muda mfupi isiyotunzika kwa mfano hela jua atazitumia zitaisha utakuwa hujajenga misingi imara wa mahusiano.

KUMBUKA: Simaanishi kuwa usimpe rafiki, ndugu au jamaa au mpenzi wako hela hapana ila inabidi ufahamu kuwa pesa hutumika katika kukidhi mahitaji na sio katika kuboresha mapenzi.

FAMILIA

kama tunavyofahamu kuwa familia ni kundi la watu wanaokaa pamoja kama Baba, Mama na watoto ambapo hupelekea kuwepo kwa ukoo mkubwa. Yote hayo hutokea kwa kujengwa kwa mahusiano yanayopelekea ndoa, na ndani ya ndoa huweza kutokea migogoro mbalimbali ambayo yanahitaji suluhisho, na iwapo tutapata suluhisho bora hupelekea uwepo wa matunda ambayo ni watoto ambao wataimarishwa kwa kupita Baba na Mama wakishirikiana na pande zote mbili za familia.

UTATUZI

ukweli usio pingika ni kwamba ndoa nyingi sana huvunjika kutokana na kukosekana kwa suluhisho bora la kutatua matatizo yanayojitokeza katika ndoa bila ya kuleta athari kwa wanandoa, watoto, pamoja na familia zote mbili ambazo zilisababisho uwepo wa ndoa hiyo.
hivyo basi matatizo yote yanaweza kutatulika kirahisi na zipo njia nyingi za kutatua ingawa wanandoa wengi hupendelea kuzivunja moja kwa moja ndoa zao na kuacha athari kubwa kabisa katika nyoyo zao. angalia video hii...

MIGOGORO

Kama tunavyoelewa hakuna kizuri kisicho na udhaifu ndani yake, hivyo basi matatizo au migogoro nayo huchukua nafasi yake katika ndoa zetu. ukweli usiopingika ni kuwa matatizo na migongano ya ndoa ni sehemu ya maisha kwa wanandoa ambayo huweza kuzidisha ladha ya ndoa ama kuiteketeketeza ndoa hiyo moja kwa moja.
kimazowea tu tunakuta kwamba chanzo kikubwa cha matatizo katika ndoa ni wivu ambao umehalalishwa katika dini ya kiislamu ila ukipita mpaka husababisha mfarakano baada ya maelew.
pia ukosekanaji wa kipato, chuki katika familia na mambo mengineyo mfano wa video yetu hii

NDOA ZA KIISLAMU

Hizi ni ndoa ambazo zinafata sheria ya kiislamu na maagizo ya mtume wetu Muhammad (s.a.w ambazo hukamilika au hufungwa baada ya kutolewa mahari kutoka uupande wa mwanamme anayetaka kuoa.

AINA ZA NDOA NA HUKUMU ZAKE



Katika makala hii fupi inshaAllaah tutajaribu kuzitambulisha aina za ndoa na kuweza kuzijua hukumu zake kisheria pamoja na maelezo kwa ufupi.
Ndoa ni mkataba unaofungwa na wanandoa kuhalalisha kila mmoja wao kuweza kustarehe na mwengine kwa mujibu wa sheria.
Ndoa ni miongoni mwa alama na miujiza yake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na ina dalili ya kuthibitika kwake katika Qur’aan na katika Sunnah.
Katika Qur’aan
Suuratu Nnisaa/3
 وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم
“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.”

Suuratu Nnuur/32
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُم
“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.”


Katika Sunnah
يامعشر الشباب ، من استطاع منكم الباءة فليتزوج فإنه أغض للبصر  وأحصن للفرج ، ومن لم يستطع فعليه  بالصوم فإنه له وجاء
 أخرجه البخاري
“Enyi vijana! Mwenye uwezo wa kuisimamia ndoa na aoe kwani huko ni kuweza kuinamisha macho na kuweza kuzikinga tupu na kama hamna uwezo basi ni juu yenu kufunga kwani huko ndiko kwenye kinga.” Al-Bukhaariy
Na pia:
النكاح من سنتي ، فمن لم يعمل بسنتي فليس مني
Ndoa ni miongoni mwa Sunnah zangu na mwenye kutenda kinyume na Sunnah zangu hatokuwa pamoja na mimi. Ibn Maajah
Ili ndoa ikamilike hupaswa kutimiza nguzo, masharti pamoja na adabu zake vinginevyo inaweza kuwa miongoni mwa ndoa zenye utata katika uhalali wake.
Ndoa, kwa mujibu wa Rai za Jamhuur Ulamaa (isipokuwa Abu Haniyfah), zimegawika kwenye sehemu kuu tatu zifuatazo:
1       Ndoa sahihi iliyokamilika
Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake na kuweza kutekelezwa.
2       Ndoa Sahihi isiyokamilika
Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake lakini imeshindwa kutekelezwa.
3       Ndoa batili au fasidi
Iliyokosekana moja ya nguzo au masharti ya kusihi kwake.



Yanayopaswa kuwepo wakati wa kufungwa ndoa (Aqdi)
Ni yafuatayo
1       Kuwepo mke na mume (ambao wataweza kuisimamia ndoa na kutokuwepo vizuizi vya kuwazuia kuoana)-miongoni mwa masharti ya ndoa.
2       Ijaabu (tamko la kuoa au kuozesha) na Qabuul (tamko la kukubali) – miongoni mwa nguzo za ndoa
3       Awepo walii -miongoni mwa masharti ya ndoa
4       Wawepo Mashahidi – miongoni mwa masharti ya ndoa
Yanayopaswa kuzingatiwa
Ni yafuatayo
  • Asiwe mmoja wa wanandoa ana vizuizi vya kuwafanya wasioane ikiwa ni vya muda au vya kudumu.
  • Mkataba wa ndoa uwe wa kudumu usiwekewe muda maalum.
  • Ridhaa, chaguo na uamuzi uwe ni wa wanandoa kusiwepo kulazimishana.
  • Wasiwe wanandoa katika hali ya kuhirimia kwa ajili ya Hajj au ’Umrah.
  • Yawepo mahari.
  • Wajulikane wanaooa au kuolewa.
  • Kusiwepo mbinu za kutoitangaza ndoa na kuificha.

Ndoa batili au fasidi
1NDOA FASIDI/ BATILIIliyofisidika kwa kukosekana moja katika nguzo, masharti ya msingi ya kufungika ndoa.Ndoa hutakiwa ikamilike mambo yake yote zikiwemo nguzo masharti ya kusihi kwake ili iweze kuwa na uhalali kisheria.Haijuzu
2NDOA WAKATI WA IHRAAMUKuoa/kuolewa wakati mmeshahirimia ima kwa ibadah ya Hajj au ‘Umrah.Kuwepo katika hali ya Ihraamu ni moja katika mambo yanayomzuia mke/mume kufanya tendo la ndoa na kuoa au kuwakilishwa ndoa pia ni mambo yasiyofanywa kwa aliye kwenye Ihraamu.Haijuzu
3NDOA BILA YA WALIIKufungwa ndoa kwa kuwepo mke na mume pamoja na mashahidi lakini Walii amekosekana.Ndoa haikamiliki bila ya kuwepo kwa Walii na ni mojawapo ya nguzo za ndoa. Walii ni mwenye haki ya kumuozesha na kusimamia ndoa kwa niaba ya binti.Haijuzu kwa mujibu wa Jamhuur Ulamaa na inajuzu kwa mwanamke aliye baleghe kujiozesha kwa mujibu wa rai ya Abu Haniyfah.
4NDOA YA “WALII” ASIYEKUWA NA SIFAKufungwa ndoa kwa kutimizwa masharti yote isipokuwa walii ni mama wa binti kwa kukosekana baba na mfano wake.Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni kuwepo walii mwanamme. Kisheria walii ni mwanamme na mwanamke si miongoni mwa walii wa binti.Haijuzu
5NDOA BILA YA KUWEPO MASHAHIDIKufungwa ndoa wakiwepo mke na mume na walii bila ya kuwepo shahidi kama ilivyo ndoa ya Mut’ah au ndoa ya siriNi moja katika masharti ya kusihi ndoa kwamba lazima ishuhudishwe na mashahidi ili kuondosha dhana ya kuwepo ndoa za siri na kuondosha tuhuma na dhana.Haijuzu


Ndoa zenye utata katika kujuzu kwake
 NDOAMAELEZOSABABUHUKUMU
1NDOA YA MUT’AH (MUDA MAALUM)Hufungwa kwa muda maalum japo masaa mawili, bila mashahidi wala walii, ambapo wanandoa kuwa na haki kama wameoana.Imewekewa muda maalum na hakuna kurithiana wala kutalikiana.Haijuzu
2NDOA YA MHALILI (ALIYEACHIKA TALAKA TATU)Kuolewa mke aliyeachika talaka tatu si kwa lengo la ndoa bali kwa lengo la kuipinda sheria ili ahalalishiwe mume wa mwanzo.Mume anataka kurudiana na mkewe ambaye kamuacha talaka tatu na hivyo kumtafuta mume mwengine amuoe mkewe kwa makubaliano lakini pasipatikane tendo la ndoa kisha amuache.
Kisheria atatakiwa aolewe na mume mwengine ndoa halisi na papatikane tendo la ndoa.
Haijuzu
3NDOA ZAIDI YA WAKE WANEMume kuoa wake zaidi ya wane kwa wakati mmoja waliokubalika kisheria.Ruhusa na mipaka tuliyowekewa na sheria ni kuwa na wake wane tu kwa wakati mmoja. (Na hata kama mke  ameachika talaka rejea  na yupo katika eda basi uharamu upo pale pale).Haijuzu
4KUOLEWA NA MUME ZAIDI YA MMOJA  WAKATI MMOJAMke kuolewa na mume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja yaani kuwa na waume wawili na kuendelea.Sheria inakataza mke kuolewa na waume wengi kwa wakati mmoja kwani ni kinyume na fitrah- maumbile ya asli (Uislamu).Haijuzu
5NDOA KWENYE EDAKumuoa au hata kumposa mke aliyeachika na bado yupo katika eda na hakuwa mke wake kabla.Kuwepo kwenye eda ya aina yoyote kwa mke ni kizuizi kinachomfunga kutoweza kuolewa mpaka imalizike isipokuwa kwa mtalaka wake tu kama mke aliyeachika talaka rejea.Haijuzu
6NDOA KWENYE UJA UZITO KWA MWANAMKE AMBAYE HAJAPATA KUOLEWA KABLAKwa mwanamke ambaye hajaolewa akazini na kupatikana ujauzito na kutaka kuolewa katika hali hii. Ndoa hizi hufanyika pale mambo yameshaharibika na kutaka kusitirianaUjauzito utakuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Ahmad na Abu Haniyfah). Uja uzito hautokuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Maalik na ash-Shafi’iy).Haijuzu kwa rai ya Ahmad na Abu Haniyfah
Inajuzu kwa rai ya Maalik na ash-Shafi’iy ila tu hatopaswa kustarehe naye mpaka ajifungue.
7NDOA KWENYE UJA UZITO KWA ALIYEACHIKAMke aliyeachika na ni mja mzito na kutaka kuolewa na mume mwengine asiyekuwa mtaliki wake.Mke aliyeachika katika uja uzito yupo katika Eda na humalizika atakapojifungua na kumaliza muda wake wa Nifasi. Kisheria Eda  inamfunga mke  kuolewa mpaka imalizike.Haijuzu
8NDOA KWA ASIYEKUWA MUISLAMU WALA HAKUTEREMSHIWA KITABU

Kuoa washirikina  na makafiri ambao si miongoni mwa walioteremshiwa vitabu kama mayahudi na manasara.Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni Uislamu. Hivyo kuoa asiyekuwa Muislamu huifanya ndoa kuwa fasidi.Haijuzu
9NDOA KWA ASIYE MUISLAMU LAKINI NI MIONGONI MWA WALIOTEREMSHIWA KITABUWalioteremshiwa vitabu miongoni mwa mayahudi na manasara na wanaowafuata katika mila zao.Uislamu ni moja ya masharti ya kusihi ndoa ila kwa mujibu wa aya za Qur’aan wameruhusika kuolewa.Inajuzu ingawa ni Makruuh – haipendezi
10KUOLEWA MUISLAMU NA ASIYEKUWA MUISLAMUMwanamke wa Kiislamu kuolewa na kafiri, mwenye kumshirikisha Allaah pamoja na mayahudi na manasara.Ndoa hulazimisha utiifu wa mke kwa  mumewe na hivyo kuwepo khofu ya kuweza kuathirika na kubadilisha dini na watoto kufuata dini ya baba.

Haijuzu
11KUOA/KUOLEWA NA ALIYERTADIMwanamme au mwanamke aliyekuwa Muislamu kisha akaamua kurtadi – kutoka katika dini.Kwa kukosekana sharti la msingi la Uislamu na hata kama atakuwa amekwenda katika dini ya walioteremshiwa vitabu.Haijuzu
12KUMUOA BINTI ULIYEZAA NJE YA NDOAMwanamme kuoa binti aliyezaa baada kutembea (kuzini) na mama yake nje ya ndoa.Huyu ni mtoto wake kwani ni mbegu zake ila tu atakosa baadhi ya haki za kimsingi kwa kuzaliwa nje ya ndoa.Haijuzu
13KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HARAMU NA MAMA YAKEKuoa binti wa kambo ambaye mliwahi kuwa na uhusiano haramu (zinaa) na mama yake kabla. Si binti aliyezaa nje ya ndoa bali ni binti wa mama.Kutokana na kupatikana tendo la haramu la zinaa Maulamaa wametofautiana katika tendo hili (zinaa) je llitaweza kuharamisha halali (ndoa)? Na kuna Qaaidah-“Haramu haiwezi kuifanya halali nyengine kuwa haramu”. Kuna Qaaidah nyengine “tendo la haramu huharamisha halali”.

Inajuzu kwa rai ya ash-Shaafi’iy na Maalik kwa sababu ya kutokuwepo dalili bayana kuharamisha. Haijuzu kwa rai ya Abu Haniyfah na Ahmad bin Hanbal kwa sababu ya kuwepo tendo la haramu zinaa.
14KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HALALI NA MAMA YAKEKuoa binti wa kambo ambaye kuliwahi kuwepo mahusiano ya halali (ndoa) na mama yake mzazi na binti huyu si miongoni mwa watoto wa mume.na Qaaidah – msingi wa kisheria yakipatikana maingiliano kwa mama huharamisha (kuolewa) binti yake.

Haijuzu

15KUOA MAMA AMBAYE ULIWAHI KUOA BINTI YAKEKumuoa mama ambaye kabla mliwahi kuwa na uhusiano wa ndoa na binti yake.Haijuzu
16NDOA KWA WALIONYONYA ZIWA MOJAIkiwa watoto wa kike na wa kiume wametokezea kunyonya ziwa moja kwa mama mmoja na wakataka kuoana.Moja katika mambo yanayoharamisha ndoa ni kuoa /kuolewa na mliyenyonya ziwa moja kwani kitendo hiki tayari kisheria kimeshaunda udugu baina yao.Haijuzu
17NDOA YA KUBADILISHANA (SHIGHAAR)Mwanamme kumuozesha binti/dada yake kwa mwanamme mwengine ambaye naye atamuozesha binti/dada yake kwa mwanamme wa mwanzo kwa mabadilishano.Ndoa hizi hufanyika pasi na kutajwa mahari kwani mahari ya kila mmoja ni kumkubalia mwengine kuoa kwake “nipe nikupe” na pasi na kupatikana ridhaa ya upande mwengine.Rai yenye nguvu haijuzu kwa kufanyika kinyume na misingi ya ndoa ya Kiislamu.
18NDOA YA BOMANINdoa zinazofungishwa na wakuu wa wilaya au kwenye ofisi za wasajili wa ndoa serikalini.Hufanyika bila ya kutekelezwa masharti ya kimsingi katika sheria za ndoa za Kiislamu kwani si lazima kuwepo mashahidi au kuwa wanandoa ni wa dini moja.Haijuzu.

Ikiwa taratibu za nchi zinahitaji kufungwa ndoa hii itawajibika kwanza kufungwa ndoa ya Kiislamu.
19NDOA YA MISYAARMwanamke hukubali kuolewa huku akisamehe baadhi ya haki zake za kimsingi katika ndoa kama mahari, huduma na makaazi au hata katika kugawana siku (kwa wake wenza).Ndoa hizi hufanyika sana katika Bara Arabu hasa kutokana na ughali wa mahari na hivyo mke katika kutafuta stara huzisamehe baadhi ya haki zake.
Na pia kama wenye kuoa Afrika huku wakiwa na mke mwengine na hivyo mke wa Afrika kusamehe baadhi ya haki zake kama za kugawana siku na nyenginezo kwa kuwa anapata huduma nyengine kama pesa na kadhalika.
Itajuzu ikiwa  imetimiza masharti ya kimsingi – Haitojuzu ikiwa haitotimiza masharti ya kimsingi kama kufanyika ndoa ya Misyaar bila ya Walii.
20NDOA YA MISFAARHufungwa kwa muda maalum kama wakati wa mapumziko au kwa wafanyakazi, wanafunzi ambao wako mbali na miji au nchi zao humalizika baada ya kurudi sehemu zao walikotokaKimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria kama ilivyo Mut’ah. Mfano wanandoa wamekubaliana kuoana wakiwa Uingereza tu lakini wakirudi walipotoka ndoa imemalizika hata bila ya talaka.Haijuzu kwa rai ya Jamhuur
Licha ya kutimiza masharti yote ya kimsingi ila kwa kuwepo muwafaka wa kumalizika kwake ambao ni kinyume na taratibu za ndoa ya Kiislamu.
Itajuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa sharti la kumalizika halitozingatiwa kwani ni sharti batili.

21KUOA MWANAMKE ALIYEPOSWA KABLAKuvunja uchumba uliopo na kuposa kisha kumuoa binti ambaye tayari ameshachumbiwa.Kwenda kuposa mwanamke aliyeposwa ni haramu kisheria. Kwa mujibu wa Hadithi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Ikiwa atakayeposa anajua taarifa za kuposwa kwa binti kabla basi
mtendaji ni mwenye madhambi na dhimma kwa kukiuka makatazo.
Kama hakujua na kufahamu baadae basi uharamu upo pale pale
Ndoa itajuzu kwa mujibu wa rai ya Jamhuur Ulamaa kwa sababu kilicho haramu kilitokea kabla ya kufungwa na si katika ndoa kwani khutba si miongoni mwa mwa masharti ya kusihi ndoa.

Haijuzu kwa mujibu wa Maalik na kama ndoa itafanyika itabidi ibatilishwe

22NDOA YA KUJIFICHA  “SIRI”Kuoana kwa kukamilisha nguzo na masharti yote ya ndoa ila tu wanandoa na mashahidi kutakiwa kutoitangaza na kuidhihirsha.Ikiwa ndoa hii itakamilika katika idara zote ila kilichokosekana ni mashahidi tu kuitangaza ndoa. Kama kuoa mke wa zaidi ya mmoja bila ya kumtaarifu mke/wake/watu wengine.Inajuzu kwa sababu ndoa imekamilika kuwepo mashahidi kumeifanya si siri tena, imeshatangazwa. Ila ni jambo lisilopendeza kisheria (makruuh)
24KUOA KWA  NIA YA KUACHAMume kuoa na katika mkataba wa ndoa akashurutisha kwamba atamuacha mke katika muda fulani au bila ya kushurutisha lakini tayari ameshaweka nia katika nafsi yake ya kuacha.Kimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria ikiwa imeshurutishwa au kuwekwa nia kwani inakuwa ndoa ya muda maalum. Na kuwepo ndani yake hadaa na udanganyifu.Haijuzu kwa rai ya Jamhuur kwa sababu ya kuwekewa muda wa kumalizika na udanganyifu.

Itaweza kujuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa shurti litabatilishwa na kutenguliwa



Ni muhimu kwa kila Muislamu kuzifahamu vyema aina hizi na kuhakikisha ndoa yake imefungwa katika misingi na taratibu zilizo sahihi. Na kama ni miongoni mwa watakaosimamia au kuwakilisha katika ndoa wazingatie maelezo haya ili waweze kuwa na uelevu katika mwenendo mzima wa ndoa kuepuka matatizo na kuepukana na ndoa zenye utata.
Pia kuwepo tayari kuusimamia ukweli na haki pale ambapo ndoa iliyofungwa ilifungwa katika misingi isiyokuwa sahihi au baadhi ya taratibu zake kukiukwa.
Ikiwa ndoa ni moja katika alama zake Allah Subhaanahu Wata’ala na miujiza yake hatuna budi Waislamu kuhakikisha kuzithibitisha alama hizi kwa kuifunga katika misingi na taratibu sahihi za kisheria.
Na Allah Ndiye Ajuaye zaid
i

Category 1

Search This Blog

Comments

DABII

MTUNZI

Pages

Popular Posts